Mkuu wa operesheni katika Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Lucas Mkondya amewataka wananchi wa mkoa huo kutoshiriki maandamano ya aina yoyote ambayo yako kinyume na sheria, kwani jeshi hilo limejipanga kudhibiti maandamano hayo.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika Makao Mkuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Mkoa kilichopo Ukonga katika Manispaa ya Ilala.
Kauli hiyo ya Mkondya imekuja baada ya Makonda kuwataka askari hao kuhakikisha wanapambana na vurugu zozote zinazoashiria uvunjifu wa amani ikiwemo maandamano yanayotarajiwa kufanyika ya UKUTA yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kuhakikisha mkoa unabaki kuwa na amani.
“Kumekuwa na maagizo yanayotolewa na wanasiasa kuhusu uwepo wa maandamano, lakini ni vyema wananchi wakapuuza na kuepuka kujihusisha na maandamano hayo kwani askari hao wamejipanga kudhibiti”, alisema.
“Tumejiandaa vizuri tumeyasikia maandamano ya UKUTA niwatahadharishe tu wananchi msidanganywe mkakubali kufanya maandamano tumejipanga, tutawashughulikia hatuna mchezo ni lazima wananchi mtii sheria bila kushurutishwa,” alilisitiza Mkondya.
No comments:
Write comments